Mabingwa wa Germany Bayern Munich wakiwa kwao Uwanjani Allianz Arena Jijini Munich Nchini Germany wameitandika FC Porto Bao 6-1 katika Mechi ya Marudiano ya Robo Fainali ya UEFA CHAMPIONZ LIGI na kutinga Nusu Fainali kwa kishindo.
Katika Mechi ya Kwanza iliyochezwa Wiki iliyopita huko Porto, Ureno, FC Porto ilishinda 3-1 lakini kipondo hiki cha huko Munich kimewatupa nje kwa Jumla ya Bao 7-4.
Bao la kwanza la Bayern lilifungwa Dakika ya 14 kwa Kichwa na Thiago kufuatia kazi safi ya Gotze na Bernat aliemimina Krosi safi na kuunganishwa wavuni na Thiago Alcantara.
Bayern walifunga Bao lao la Pili Dakika ya 22 baada ya Kona kupigwa Kichwa na Badstuber na Jerome Boateng kumalizia kwa Kichwa kingine na kuwafanya Mabingwa wa Germany wawe 2-0 mbele.
Dakika ya 27, Lewandowski akaipeleka Bayern 3-0 mbele baada ushirikiano mzuri wa Nahodha Lahm na Muller na kisha Robert Lewandowski kumalizia vizuri kwa Kichwa.
Thomas Muller aliipa Bayern Bao la 4 katika Dakika ya 36 baada ya Shuti lake dhaifu kumbabatiza Beki Martins Indi na kumhadaa Kipa Fabiano.
Dakika ya 40, Lewandowski aliifanya Bayern iwe 5-0 mbele baada ya Kona kunaswa na Lahm na Muller kucheza vizuri na kumfikia Lewandowski aliemalizia vyema.
Hadi Mapumziko, Bayern 5 FC Porto 0.
Dakika ya 73 Jackson Martinez aliifungia FC Porto Bao 1 akiwa wazi Ofsaidi na Gemu kuwa 5-1.
FC Porto walipata pigo Dakika ya 87 baada ya Marcano kupewa Kadi ya Njano ya Pili na kutolewa nje kwa Kadi Nyekundu baada ya rafu yake kwa Thiago na kuzaa Frikiki toka Mita 25 ambayo Alonso alifunga na Bayern kuwa mbele Bao 6-1.
Jumatano Usiku zipo Mechi nyingine mbili za Robo Fainali na Juventus, walioshinda kwao Turin, Italy Bao 1-0, wako Ugenini kurudiana na AS Monaco na pia ipo Bigi Mechi, El Derbi Madrileno, Dabi ya Jiji la Madrid, wakati Mahasimu Real Madrid na Atletico Madrid watakaporudiana huko Santiago Bernabeu huku matokeo ya Mechi ya kwanza yakiwa ni 0-0.
Droo ya kupanga Mechi za Nusu Fainali itafanyika Ijumaa Aprili 24 huko Nyon, Uswisi na Mechi zake zitachezwa Mei 5 na 6 na Marudiano hapo Mei 12 na 13.
0 comments:
Post a Comment