Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro sasa itaondoka nchini siku ya jumapili usiku kuelekea Istambul nchini Uturuki kwa kambi ya siku nane kujiandaa na mchezo dhidi ya Nigeria Septemba 05, 2015.
Awali Taifa Stars ilikua ipitie Muscat nchini Oman kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya taifa ya nchi hiyo, lakini kutokana na shirkikisho la Soka la Oman kushindwa kukidhi mahitaji ya Kanuni za FIFA za uuandaaji wa mechi ya kimataifa ya kirafiki sasa mchezo huo hautakuwepo tena.
Stars inatarajiwa kuondoka jumapili usiku na shirika la ndege la Uturuki (Turkish Airlines) na kuwasili Istambul (Ataturk Airport) siku ya jumatatu majira ya saa 5 kamili asubuhi, kisha kuelekea Kocael katika hoteli ya Green Park Kartepe ambapo ndio itakua kambi yake ya wiki moja.
UCHAGUZI WA TEFA WAAHIRISHWA
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi Aloyce Komba imeitisha majalada ya kamati ya uchaguzi ya TEFA na kamati ya uchaguzi ya DRFA baada ya kupokea malalamiko na rufaa kutoka kwa wagombea.
Kamati ya Uchaguz ya TFF imeyaomba majalada hayo ili ijiridhishe na kuona haki inatendeka kwa wagombea wote na baadae tarehe mpya ya uchaguzi itatolewa.
SAANYA KUCHEZESHA AZAM NA YANGA
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limemteua mwamuzi wa kati Martin Saanya kuchezesha mchezo wa Ngao ya Jamii jumamosi, badala ya mwamuzi Israle Nkongo aliyekua amepangwa awali.
Mwamuzi Israel Nkongo anasumbuliwa na matatizo ya misuli ya paja, ambayo itampelekea kukaa nje ya uwanja kwa takribani siku kumi, hali iliyopeleka TFF kumbadilisha mwamuzi huyo kuelekea kwenye mchezo huo wa jumamosi.
KIKOSI CHA U-13 CHATANGAZWA
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limetangaza kikosi cha timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 13 (U13) kitakacho kuwa jijini Mwanza kujiandaa na fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 mwaka 2019 nchini Tanzania.
Mapema mwezi Juni mwaka huu TFF iliandaa mashidano ya Taifa ya vijana yaliyofanyika jijini Mwanza ambapo japo la makocha chini ya Idara ya ufundi ya TFF, waliweza kuchagua vijana wenye vipaji ambao wanaunda timu hiyo.
Vijana hao wenye vipaji watakua wakiishi, kufundishwa mpira na kusoma katika shule ya Alliance iliyopo jijini Mwanza ambayo TFF imeingia mkataba na shule hiyo kwa ajili ya kuwalea wachezaji hao na kuendeleza vipaji vyao.
Mpango huo wa kuandaa kikosi cha vijana utafanyika pia mwakani kwa kuchagua vijana wenye umri chini ya miaka 14 (U14), na mwaka unaofuata kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 (U15) kwa lengo la kuendelea kuboresha kikosi hicho cha vijana.
Wachezaji waliochaguliwa kujiunga na timu hiyo ya vijana ni Jaffar Juma (Arusha), Moris Michael (Ilala - Dsm), Jonathan Raphael (Kasulu – Kigoma), Karim Mfaume (Lindi), Erick Buyaga (Nyamagana – Mwanza), Shabani Kimwaga (Kinondoni – Dsm), Feisally Awadh (Ilala – Dsm), Abdulatif Noor (Tanga), Edmond Godfrey (Geita) na Adam Selemani (Kibaha – Pwani).
Wengine ni Selaman Juma (Kibaha – Pwani), Wilbert John (Ilala – Dsm), Ahsante Hamisi (Kinondoni – Dsm), Isaya Ernest (Mbeya), Gasper Gombanila (Nyamagana – Mwanza), Joseph Awadh (Ilala – Dsm), Alfonsi Mabula (Nyamagana - Dsm), Cosmas Lucas (Nyamagana – Mwanza), Haroub Juma (Bariadi – Simiyu) na Ladak Juma (Morogoro).
Wakati huo huo wachezaji watano kutoka kikosi cha timu ya Taifa cha vijana wenye umri chini ya miaka 15 (U15) wanatarajiwa kuondoka nchini mwishoni mwa mwezi huu wa Agosti kuelekea nchini Afrika Kusini kwa ajili ya majaribio katika klabu ya vijana ya Orlando Pirates.
Nafasi hiyo imepatikana kufuatia mazungumzo ya Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Rais wa klabu hiyo Irvin Khoza kuomba vijana hao kupata nafasi ya kufanya majaribio katika klabu hiyo na endapo watafuzu, watajiunga na timu ya vijana ya Orlando Pirates.
Wachezaji hao ni Asaad Ali Juma (Zanzibar), Maziku Amaan (Dodoma), Issa Abdi (Dodoma), Kelvin Deogratias (Geita) na Athumani Maulid (Kigoma) wataongozana na Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi kuelekea Afrika Kusini Agosti 28, 2015 kwa ajiliya kufanya majaribio hayo.
BY: Baraka Kizuguto
MEDIA & COMMUNICATION OFFICER
TFF
0 comments:
Post a Comment