Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara inatarajiwa kuendelea kesho kwa mchezo mmoja utakaopigwa katika dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, wenyeji timu ya Azam FC watawakaribisha Mabingwa wapya wa ligi hiyo msimu huu timu ya Young Africans.
Mechi hiyo no. 141 itachezeshwa na mwamuzi wa kati Jacob Adongo kutoka Mara, akisaidiwa na washika vibendera Frednand Chacha (Mwanza), Hellen Mduma (Dsm), huku mwamuzi wa akiba akiwa ni Hussein Kalindo (Dsm) na Kamisaa wa mchezo huo ni Damian Mabena kutoka Tanga.
Katika mchezo huo timu ya Young Africans itakabidhiwa Kombe lake la Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara msimu wa 2014/2015, na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dr Fennela Mkangara.
Mchezo huo wa kesho unatarajiwa kuanza majira ya saa 11 kamili jioni, kwa saa za Afrika Mashariki na kati ili kutoa fursa kwa wadau, wapenzi na mashabiki wa mpira wa miguu nchini kujitokeza kushudia mchezo huo pamoja na shamrashamra za kukabidhiwa kikombe.
Young Africans watakabidhiwa Kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu na mgeni rasmi, huku wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom wakimkabidhi zawadi mchezaji bora wa mwezi Aprili Mrisho Ngasa na fedha taslimu sh. millioni moja.
0 comments:
Post a Comment