Mechi tatu za ligi kuu vodacom zitapigwa leo Prisons dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Sokoine, Ruvu Shooting itapambana na Coastal Union (Mabatini) na Polisi Moro itakabiliana na JKT Ruvu (Jamhuri).
Mechi yenye mvuto mkubwa ni ile ya Simba na Mtibwa Sugar itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mechi hiyo inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na rekodi mbalimbali za timu hizo msimu huu ambapo katika mchezo wa kwanza uliozikutanisha mjini Morogoro, zilitoka sare ya bao 1-1 na hata kwenye fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyofanyika visiwani Zanzibar, Simba ilishinda kwa penalti 8-7.
Kikosi cha Simba kinachofundishwa na Mserbia, Goran Kopunovic, kitashuka katika mechi hiyo kikiwa na kumbukumbu ya kushinda michezo miwili iliyopita ambayo ni dhidi ya Prisons (5-0) na Yanga (1-0).
Simba sasa hivi wapo nafasi ya tatu kwenye msimamo wakiwa na alama 26 huku Mtibwa wakiwa na pointi 23, nafasi ya tano.
KAULI YA KOPUNOVIC.
“Itakuwa ni mechi ngumu kwani Mtibwa Sugar siyo timu mbaya lakini nimeshawaandaa vijana wangu kiufundi na kisaikolojia kuhakikisha wanapambana ili tuweze kupata ushindi.”
KAULI YA MECKY MEXIME
“Sina mengi ya kuongea juu ya mechi hiyo ila jambo la msingi ni kwamba tutaingia uwanjani kupambana ili tuweze kuibuka na ushindi kwani na sisi tunazihitaji hizo pointi tatu.”
0 comments:
Post a Comment