Coutinho na Nahodha wa timu hiyo Nadir Haroub ‘Cannavaro’ hawatoshiriki mchezo huo wa awali kutokana na majeruhi yanayowakabili mpaka sasa
KIUNGO wa Yanga raia wa brazili Andrew Coutinho, ataukosa mchezo wa pili wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika CAF, dhidi ya FC Platnam ya Zimbabwe kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu aliyoyapata wiki tatu zilizopita katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mbeya City.
Daktari wa Yanga Juma Sufian amesema Coutinho na Nahodha wa timu hiyo Nadir Haroub ‘Cannavaro’ hawatoshiriki mchezo huo wa awali kutokana na majeruhi yanayowakabili mpaka sasa.
“Coutinho aliumia kwenye mechi ya ligi dhidi ya Mbeya City, na amekosa mechi ya marudiano dhidi ya BDF XI, ya Botswana na atakosa mechi ya kwanza dhidi ya Platnam pamoja na Cannavaro ambaye amepasuka kwenye paji la uso kwenye mchezo dhidi ya Simba Jumapili iliyopita,”amesema Juma Sufiani.
Yanga Jumapili itashuka kwenye uwanja wa taifa Dar es Salaam kuikabili FC Platnam ya Zimbabwe, ambayo inawasili Tanzania leo jioni kwa ajili ya pambano hilo la raundi ya pili michuano ya CAF.