Zikiwa zimebaki chini ya Siku 40 kabla Manchester United hawajaanza kucheza Msimu mpya wa 2015/16, Wachezaji wa Timu ya Kwanza wameaanza kurejea Kituo cha Mazoezi cha Carrington Jijini Manchester.
Timu hiyo itaruka hapo Julai 13 kwenda Marekani kwa ajili ya Ziara kabla Msimu kuanza na kucheza Mechi na Club America, San Jose Earthquakes, Barcelona na Paris Saint-Germain.
Man United watafungua Msimu wao mpya wa Ligi Kuu England hapo Agosti 8 Uwanjani Old Trafford kwa kucheza na Tottenham.
Benchi la Ufundi likiongozwa na Meneja Louis van Gaal, Msaidizi wake Ryan Giggs na Wasaidizi wengine wameandaa programu kabambe kuwatayarisha Wachezaji hao.
Safari hii Van Gaal ameandaa programu spesho ili kuepuka mwanzo mbovu alioupata Msimu uliopita ambao ulikuwa Msimu wake wa kwanza ambapo walifungwa Mechi ya kwanza na Swansea na kuambua Pointi 13 tu katika Mechi zao 10 za kwanza.
Lakini si Wachezaji wote wamesharejea huko Carrington kwani Wayne Rooney, Robin van Persie na Wawili ambao wapo na Argentina kwenye Copa America, Angel Di Maria n Marcos Rojo, bado kujumuika na wao wamepewa muda zaidi wa kupumzika kutokana na kuwa na Timu zao za Taifa.
Mchezaji mwingine ambae anategemewa kuwa kundini ni mpya Memphis Depay alienunuliwa toka Uholanzi Klabu ya PSV Eindhoven.
Wachezaji 9 ambao walikuwa nje kwa Mkopo Msimu uliopita nao wamerejea na hao ni Sam Johnstone, Reece James, Guillermo Varela, Jesse Lingard, Nani, Angelo Henriquez, Javier Hernandez na Will Keane.
Kitu cha kwanza kabisa hukabiliwa nacho Wachezaji hao baada kurudi kazini ni kupimwa Afya zao na kisha kulivaa Jopo maalum la Wasaidizi wa Van Gaal ambao ni Wataalam toka Idara ya Sayansi ya Michezo akiwepo Jos van Dijk, ambae amekuwa na Van Gaal kwa Miaka 8 sasa, ambae jukumu lake ni kumtayarishia kila Mchezaji Mazoezi maalum binafsi.
Akiongelea Ziara ya USA, Van Gaal ameeleza: "Katika Mechi 2 za kwanza, nitachezesha Wachezaji wote kwa Dakika 45 ili wazoee hali mpya. Wamekuwa vakesheni kwa Wiki 3 au zaidi na hiyo ni kuwapa nafasi kurejea hali ya kawaida. Chipukizi wengi watapata fursa kucheza."
0 comments:
Post a Comment